Kuorodhesha hisa za kampuni yangu DSE?

Mchakato wa kuorodhesha hisa huhitaji mwongozo wa kitaalam. Kanuni za Mamlaka (CMSA) na Soko la Hisa la Dar-es-Salaam (DSE) zinaelekeza kuwa kila anayetaka kutoa hisa au hatifungani kwa umma inabidi ateue dalali mdhamini au mshauri mteule kwa ajili ya kudhamini toleo hilo jipya au kuorodheshwa. Dalali mdhamini au mshauri mteule ataisaidia kampuni katika kutimiza masharti yanayotakiwa kwa kuzingatia mambo mbalimbali kama vile iwapo hisa za kampuni husika tayari ziko kwenye mikono ya umma au ni hisa mpya. Dalali mdhamini ataiongoza kampuni inayotaka kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa kwenye safu kuu ya soko la hisa (MIMS); na mshauri mteule ataiongoza kampuni inayotaka kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa kwenye safu ya soko la kukuza kampuni na ujasiriamali ya soko la hisa(EGM). Aidha kampuni zinazotaka kuuza hisa kwa umma na hatimaye kuorodheshwa katika safu hizi mbili, zinatakiwa kuwa na sifa fulani na kutimiza masharti yaliyoainishwa na Sheria ya Masoko ya Mitaji na dhamana na taratibu za Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Kukusanya Mtaji kwa Umma na Kuorodheshwa kwenye Safu Kuu ya Soko la Hisa (Main Investment Market Segment (MIMS))

Masharti

  1. Kampuni iwe imeandikishwa Tanzania chini ya sheria ya kampuni kama kampuni ya Umma na kuwa na wanahisa wasiopungua 7;
  2. Kampuni iwe na uzoefu usiopungua miaka mitatu na kuwa na mahesabu yaliyokaguliwa ya miaka mitatu;
  3. Kampuni iwe na mtaji wa kufanyia kazi (working capital) wa kutosha;
  4. Kampuni iwe na historia ya kupata faida ya miaka miwili kati ya miaka mitatu wakati wa kuleta maombi ya kuorodheshwa;
  5. Hisa zake ziwe zinahamishika bila kikwazo;
  6. Ikubaliane na masharti ya kudumu ya kuwepo kwenye soko la hisa;
  7. Angalau 25% ya hisa zake ziwe mikononi mwa umma;
  8. Kampuni iwe na mtaji angalau TZS milioni 200;
  9. Kampuni iwe na angalau wanahisa 1000; na
  10. Inatakiwa kuonyesha kuwepo na bodi na uongozi thabiti.

Zingatia: Iwapo kampuni inayoomba kuorodheshwa kwenye soko la hisa ni ya kigeni inatakiwa iwe imeandikishwa Tanzania kama kampuni ya kigeni.

Utaratibu wa Kujiorodhesha

  1. Kupata ridhaa ya kuuza hisa kwa umma kutoka kwa wanahisa;
  2. Kuteua timu ya wataalamu watakaoitayarisha kuingia kwenye soko la hisa;
  3. Kutayarisha waraka wa matarajio kama inavyotakiwa na kanuni za utayarishaji wa waraka wa matarajio;
  4. Kuteua dalali mdhamini;
  5. Kuwasilisha kwa Mamlaka (CMSA) na Soko la Hisa (DSE), maombi ya kuorodhesha hisa na dhamana kwa kupitia kwa dalali mdhamini;
  6. Kupata kibali kutoka kwa Mamlaka na Soko la Hisa ili kuanza kuuza hisa katika soko la awali.

Kukusanya Mtaji kwa Umma na Kuorodheshwa kwenye Soko la Kukuza Ujasiriamali (Enterprise Growth Market, (EGM))

Masharti

Yafuatayo ni masharti kwa kampuni inayoomba kukusanya mtaji kwa umma kwa kuuza hisa na kuorodheshwa katika safu ya EGM:

1.Lazima iwe imesajiliwa kama kampuni ya Umma(Public Limited Company) chini ya Sheria ya kampuni;

2.Hakuna kiwango maalum cha mtaji kinachotakiwa;

3.Historia ya utendaji kazi haihitajiki;

4.Historia ya upatikanaji faida haihitajiki;

5.Kama kampuni haitakuwa na historia ya utendaji kazi, waanzilishihawataruhusiwa kuuza hisa zao katika muda wa miaka mitatu ya mwanzo baada ya kampuni kuwa imeorodheshwa;

6.Kampuni lazima iwe na Mshauri Mteule;

7.Lazima iwe na mpango wa biashara wa miaka mitano na taarifa ya ufundi ya kujitegemea iliyotayarishwa na Mshauri Mteule kuhusiana na matarajio ya upatikanaji faida;

8.Kiwango cha chini cha wanahisa ni 300;

9.Umiliki wa umma kwenye kampuni iliyo kwenye soko hili unatakiwa usipungue 20% ya hisa zilizotolewa;

10.Lazima kutengeneza Waraka wa Matarajio na upitishwe na Mamlaka;

11.Waraka wa Matarajio kwa Ufupi uwekwe kwenye magazeti;

12.Lazima kuwe na Kamati ya Ukaguzi kama mwongozo wa utawala bora wa kampuni unavyotaka;

13.Katiba na Waraka wa kuanzishwa kwa kampuni inabidi itamke ulazima wa kufuata misingi ya utawala bora wa kampuni.

Utaratibu:

Kampuni ambayo imetimiza masharti ya mwanzo ya kuorodheshwa inabidi ifuate utaratibu ufuatao:

1.Kuteua timu ya wataalam washauri (consultants) kuiandaa kampuni kwa ajilikuuza hisa kwa umma na kuorodhesha hisa hizo kwenye soko la hisa;

2.Kuteua Mshauri Mteulekuisimamia kampuni tangu wazo la kutafuta mtaji linapokuja hadi kuirodhesha kwenye soko la kukuza ujasiriamali;

3.Kutengeneza Waraka wa Matarajio kwa ajili ya kuuza hisa kwa umma kama inavyotakiwa na kanuni za Mamlaka na Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana;

4.Kampuni inabidi ibakie na Mshauri Mteule kwa kipindi chote ambacho kampuni itakuwa imesajiliwa kwenye soko;

5.Inabidi kuwasilisha kwa Mamlaka (CMSA) nasoko lahisa (DSE) maombi ya kuuza hisa na kuorodheshwa kwenye soko la hisa; na

6.Kupitishwa kwa Waraka wa Matarajio kunaiwezesha kampuni kuanza kuuza hisa zake kwa umma kama ilivyoelezwa hapo juu kwenye soko la awali.

Gharama za Kushiriki kwenye Soko la Kukuza Ujasiriamali

Gharama za ushiriki katika EGM zinahusisha ada za kulipa wataalamu mbali mbali watakoongoza kampuni katika mchakato huo. Wataalamu hao ni pamoja na Mshauri Mteule, Mhasibu, Mwanasheria, Mshauri Mkuu na Wakala wa Matangazo na Uchapishaji wa Matangazo na Toleo. Ada zao hamna viwango maalumu ila ni makubaliano kati yao na kampuni husika. Ada za kuchambua waraka wa toleo za CMSA na ada ya kuorodheshwa DSE zimeainishwa kwenye jedwali hapo chini. Ada hizi zimewekwa nafuu kabisa ili kupunguza mzigo kwa kampuni zinazotarajia kutumia EGM kupata mtaji na kuorodheshwa.

Ada ya Kupitia Waraka wa Matarajio (CMSA)

Thamani ya Mtaji

Ada

TZSbilioni 1 au chini yake

TZS 1,000,000

Kati ya TZSbilioni 1 na bilioni 5

TZS milioni1 ongeza0.1%ya kiasi kinachozidi TZS bilioni 1

Kati ya TZS bilioni 5 na 10

TZSmilioni5 ongeza0.05%ya kiasi kinachozidi bilioni 5

Zaidi ya TZS bilioni 10

TZS milioni7.5 ongeza0.025%ya kiasi kinachozidiTZS bilioni 10

Ada ya kuorodheshwa DSE

Ada ya mwanzo ya kujisajili

0.1% ya thamani ya hisa zinazo orodheshwa (kiasi cha chini TZSmilioni 1 na kiasi cha juu TZS milioni 10)

Ada ya kusajili hisa nyingine

0.1% ya thamani ya hisa zinazoongezwa (kiasi cha chini TZS milioni 1 na kiasi cha juu TZS milioni 10)

Ada kwa kila mwaka

0.025% ya thamani ya hisa(kiasi cha chini TZSmilioni 1 na kiasi cha juu TZS milioni 10)

Kupitishwa kwa waraka wa matarajio kutairuhusu kampuni kuanza kuuza hisa kwa umma kwenye soko la awali.

Kwa taarifa zaidi pakua