Maswali Yaulizwayo Mara kwa Mara
Mchakato wa kuorodhesha hisa huhitaji mwongozo wa kitaalam. Kanuni za Mamlaka (CMSA) na Soko la Hisa la Dar-es-Salaam (DSE) zinaelekeza kuwa kila anayetaka kutoa hisa au hatifungani kwa umma inabidi ateue dalali mdhamini au mshauri mteule kwa ajili ya kudhamini toleo hilo jipya au kuorodheshwa. Dalali mdhamini au mshauri mteule ataisaidia kampuni katika kutimiza masharti yanayotakiwa kwa kuzingatia mambo mbalimbali kama vile iwapo hisa za kampuni husika tayari ziko kwenye mikono ya umma au ni hisa mpya. Dalali mdhamini ataiongoza kampuni inayotaka kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa kwenye safu kuu ya soko la hisa (MIMS); na mshauri mteule ataiongoza kampuni inayotaka kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa kwenye safu ya soko la kukuza kampuni na ujasiriamali ya soko la hisa(EGM). Aidha kampuni zinazotaka kuuza hisa kwa umma na hatimaye kuorodheshwa katika safu hizi mbili, zinatakiwa kuwa na sifa fulani na kutimiza masharti yaliyoainishwa na Sheria ya Masoko ya Mitaji na dhamana na taratibu za Soko la Hisa la Dar es Salaam.
Hapana, kwa kawaida kampuni zilizoorodheshwa huwa hazina utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanahisa wake kwa kushikilia hisa zao kama rehani. Wewe kama mwanahisa iwapo unataka fedha taslim kutokana na hisa zako kuna njia mbili. Njia ya kwanza ni kuiendea taasisi yenye kutoa mikopo na kuiomba mkopo kwa kuweka hisa zako kama rehani (hii inategemea kama unatimiza vigezo vingine vya kupewa mkopo kulingana na masharti ya benki husika). Njia ya pili ni kuuza hisa zako kwenye soko la hisa kupitia kwa dalali wa soko la hisa.
Mahali hasa pa wewe kuwasiliana unapotaka kuwekeza katika dhamana ni dalali yeyote wa soko la hisa. Madalali wa soko la hisa watakushauri na iwapo utaamua kuwekeza, watafanya hivyo kwa niaba yako. Kundi jingine unaloweza kuwasiliana nalo kwa msaada na ushauri ni washauri wa uwekezaji waliopewa leseni na Mamlaka. Washauri wa uwekezaji ambao si madalali wa soko la hisa wanaweza tu kutoa ushauri lakini hawaruhusiwi kununua hisa kwa niaba yako. Endapo unahitaji kutambua orodha yamadalali wa soko la hisa unaweza kuangalia orodha yao kwenye orodha ya Madalali wa Soko la Hisa. Aidha unaweza pia kuwasiliana na Soko la hisa au Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ili kupata orodha ya washauri wa uwekezaji.
Kwa upande wa mauzo au manunuzi ya hisa yenye kutiliwa mashaka sehemu muafaka hasa ya kutoa taarifa ni Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) au Soko la Hisa (DSE). CMSA inao wajibu wa kusimamia masoko ya mitaji na kuona kuwa biashara hii inafanyika katika utaratibu unaozingatia sheria na taratibu halali zilizopo. Vilevile mienendo yenye kutiliwa mashaka katika kuuza na kununua hisa inaweza kutolewa taarifa katika Soko la hisa la Dar-es-Salaam. Soko la hisa kama taasisi yenye kujisimamia inazo kanuni mbalimbali na utaratibu wa kuwaadhibu wanachama wake.
Hapana, uwezekano wa hasara zinaenda pamoja na umiliki. Bei ya hisa inaweza kupanda (ambapo ni jambo jema kwako kama mwekezaji) na inaweza kushuka (ambapo ni jambo baya kwako kama mwekezaji). Mashaka ya namna hii (uwezekano wa hasara) yapo tangu siku unapoamua kuwekeza kwenye hisa. Iwapo utapoteza hati yako ya hisa(kwa wale ambao bado wanamiliki / wanazo hati za hisa kwenye baadhi ya makampuni yaliyoorodheshwa kwenye soko la hisa) unashauriwa kutoa taarifa ya upotevu huo kwenye kituo cha polisi kilicho karibu ili upewe taarifa ya polisi na kuiwasilisha mara mojakwa katibu wa kampuni.
Ndiyo, kumekuwa na ongezeko la taasisi za fedha kukubali hisa hasa za kampuni zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa kama rehani kwa ajili ya kutoa mikopo. Utaratibu wa kuweka hisa au vipande kuwa rehani umedhihirisha kuwa niwenye manufaana rahisi kwa mkopaji na mkopeshaji kwa sababu inachukua muda mfupi, uko wazi, hakuna gharama za kuthaminisha na kuna uwezekano mdogo wa kufanya udanganyifu. Hatifungani za serikali, hawala za serikali na hatifungani za kampuni zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa zinakubaliwa na taasisi nyingi zinazokopesha kama rehani ya mikopo.
Mwanahisa hana usimamizi wa moja kwa moja katika uendeshaji au usimamizi wa mali za kampuni kama vile rasilimali na madeni. Uendeshaji wa shughuli za kampuni ni jukumu la Menejimenti ikisimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi. Haki za mwanahisa katika kufanya maamuzi kuhusiana na uendeshaji wa kampuni zinaishia kwenye kupiga kura katika mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa au mkutano maalum wa kuwachagua Wakurugenzi kulingana na katiba ya kampuni (MEMART). Mwanahisa ana haki ya kushiriki maamuzi ya kuteua kampuni ya kukagua mahesabu (auditors), kupitisha taarifa ya mwaka, na kupitisha mapendekezo mengine yanayohitaji kupitishwa na mkutano mkuu kulingana na katiba ya kampuni. Rasilimali za kampuni zinamilikiwa na kampuni wakati wawekezaji/wanahisa wanamiliki hisa za kampuni. Hali kadhalika, madeni ya kampuni iliyoanzishwa kwa mtaji wa hisa yana ukomo kwa kiasi mwanahisa alichowekeza na hayawezi kugusa mali binafsi za wanahisa kama kampuni ikifilisika.
Huu ni utaratibu unaotumika kimataifa. Thamani ya wanahisa inaonyeshwa au kubebwa na thamani ya hisa. Kwa hiyo, wanahisa wanapohudhuria mkutano mkuu wa mwaka au mkutano mkuu maalum wanakuwa wanatumia moja ya haki zao kuisimamia Bodi ya Wakurugenzi kwa kupitisha au kutopitisha mapendekezo mbalimbali ya Bodi. Kwa hiyo wanahisa wanapohudhuria mikutano kama hiyo hufanya hivyo kwa ajili ya kusimamia/kutetea maslahi yao kwenye kampuni. Kama kampuni ikilipa gharama za wanahisa wanapohudhuria mikutano mikuu au mikutano maalum (AGMs/ EGMs) itakuwa imeongeza gharama za uendeshaji, hali itakayo punguza faida wanayotakiwakupata wanahisa.
Hisa na dhamana nyingine ni mali kama zilivyo mali nyingine kama vile nyumba na magari. Mwekezaji akifariki, dhamana zake zinachukuliwa kama mali nyingine za marehemu kwenye mchakato mzima wa mirathi. Kama marehemu alikuwa ameacha wosia, basi dhamana hizo zitarithiwa na aliyeachiwa urithi. Kama hakuacha wosia, dhamana hizo zitagawanywa kama sheria ya mirathi inavyobainisha.